"NILIVYOANZA UFUGAJI WA NYUKI WANAOUMA NA WASIOUMA" ..SHUHUDA
Share
Ufugaji Nyuki ni miongoni mwa sekta muhimu za kiuchumi nchini Tanzania, yenye mchango mkubwa kwenye maisha ya watu wengi mijini na vijijini. Sekta hii inakadiriwa kuajiri zaidi ya watu milioni mbili nchini kwenye mnyororo wake mzima wa thamani. Mazao ya nyuki kama vile asali, nta, chavua, gundi ya nyuki, maziwa ya nyuki na sumu ya nyuki, yanatumika yakiwa kwenye hali tofauti pia kama malighafi ya viwanda vya chakula, urembo, dawa, nguo, ngozi, umeme na mishumaa. Ufugaji Nyuki umedhihirisha kuchangia ongezeko la uzalishaji wa mazao kwa kuongeza ubora wa mbegu na uhifadhi wa bioanuai kwa njia ya uchavushaji unaofanywa na nyuki. Kutokana na umuhimu kwenye uchavushaji, ufugaji nyuki umetambuliwa kama nyenzo ya uhifadhi. Pamoja na michango hii yote, bado sekta ya ufugaji nyuki haijaonekana kuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi na uzalishaji wa mazao ya nyuki kutokana na kutofuatwa kwa taratibu bora za ufugaji nyuki. Tangu kuanza kutumika kwa Sera ya Taifa ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998, ambayo inahimiza uanzishwaji na umiliki wa Hifadhi za Nyuki na manzuki ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki, kumekuwa na maendeleo yasiyolingana kwenye maeneo tofautitofauti ndani ya sekta. Mfano, hakuna maendeleo yanayoridhisha kwenye uanzishwaji wa Hifadhi za Nyuki na manzuki. Aidha, kuna zaidi ya misitu 100 inayomilikiwa na Serikali na Sekta Binafsi iliyobainishwa kuwa hifadhi za nyuki lakini haijatangazwa kwenye Gazeti la Serikali kwa kuzingatia Sheria ya Ufugaji Nyuki Na. 15 ya mwaka 2002. Hali hii inaifanya baadhi ya misitu kupoteza hadhi yake ya kutumika kama hifadhi za nyuki na kutangazwa kisheria. Kwa miaka kadhaa, wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Serikali, Asasi Zisizo za Serikali (AZISE), Asasi za Kijamii, Sekta binafsi na vijiji vimeanzisha hatua za kutangaza Hifadhi za Nyuki lakini vimeshindwa kukamilisha hatua za kutangaza hifadhi hizi kisheria.
KATIKA MAKALA MAALUM ya leo tunakuletea ushuhuda kutoka kwa mfugaji maarufu wa nyuki wanaouma na wasiouma Mr.Moh'd Rafii Yussuf mkazi wa
Donge vijibweni Mkoa wa Kaskazini Wilaya ya Kaskazini B visiwani ZANZIBAR.
HII NDIO HISTORIA NAMNA MFUGAJI HUYU ALIVYOANZA MRADI WAKE:-
"Nilianza harakati hizi mnamo machi 2013.
Kabla nilikuwa sielewi kabisa kama nyuki anafugwa.
Kwa ufupi Mimi binafsi nilikuwa mtumiaji sana wa asali kwa ajili ya tiba ya Mama watoto wangu lakini kwa bahati mbaya sana mara nyingine nilikuwa nauziwa asali feki hivyo badala ya kutibu ilikuwa ni kuongeza matatizo"
"Siku moja nilimuuliza mteja wangu ambae mara nyingi nilikuwa nikinunua asali kutoka kwake "ninavojua mimi asali ina msimu mbona wewe kila siku unayo? Unaipata wapi? “
Akanijibu kuwa ananunua, nikataka kujua kwa nani wapi.
Aliponieleza kuwa Nyuki wanafugwa nikaingia chakachani kutaka kujua ili nami niweze kjivunia Asali isiyo shaka mimi mwenyewe"
Hatimae nikapata taarifa kuwa idara ya misitu Zanzibar wameanzisha mafunzo ya ufugaji Nyuki chini ya udhamini wa shirika la ZALWEDA kutoka Denmark, ingawa nilikuwa nimechelewa lakini nilianzia katika mafunzo ya vitendo moja kwa moja ambapo nilikuta wengi wa washiriki walioanza mafunzo wameshaachia njiani eti kwa sababu tu walitegemea wawe wanalipwa na kumbe ilikuwa ni kinyume chake, "yalikuwa mafunzo bila kulipa wala kulipia" hatimae nilibaki mimi na mwalimu wangu tu.
Mwalimu wangu kwa jina la umaarufu "BARUAN" kutoka Muyuni Mkoa wa kusini Unguja alifahamu lengo langu akabaki na mimi na hadi sasa bado ananitembelea na kunifunza katika mradi wangu"
HAPA MFUGAJI ANASIMULIA NAMNA ALIVYOPATA MTAJI KWA AJILI YA UFUGAJI WA NYUKI:-
"Hili lilikuwa tatizo kubwa lakini kwa umahiri mkubwa Mwalimu wangu BARUAN alinishauri kutumia masanduku ya Tungule/nyanya ambayo ni rahisi kupatikana na mara nyingine hupatikana bila garama yoyote.Niliyavunjavunja na kuyajenga upya kwa kufuata vipimo vilivopendekezwa kwa mizinga ya Nyuki.
Baadae tena mwaka 2015 nilibahatika kupata mafunzo mengine ya Nyuki wasiouma chini ya udhamini wa shirika la ICIPE kutoka Kenya kupitia idara ya misitu Zanzibar.
Hivi karibuni tena mwaka 2023 nimebahatika tena kupata mafunzo ya uzalishaji wa mazao ya Nyuki kama vile:- Asali, Nta, Chavua, Sumu ya Nyuki, Maziwa ya Nyuki, Gundi ya Nyuki na mkate wa Nyuki.
Mafunzo haya nayo yalidhaminiwa na Wizara ya uwezeshaji Zanzibar yakiongozwa na mtaalamu wa Nyuki maarufu "kiemi" kutoka Singida, ambapo kwa sasa mimi nimeamua kuzalisha CHAVUA, ASALI NA NTA"
Mambo ambayo anazingatia mfugaji huyu:-
1) Kuchagua eneo lililo salama kwa Nyuki wenyewe na binadamu pia.
2) Mizinga ya Nyuki ifuate vipimo vilivopendekezwa.
3) Kuwa na vifaa na zana zote kwa ajili ya ufugaji Nyuki.
ZIFUATAZO NI CHANGAMOTO AMBAZO MFUGAJI HUYU ANAKABILIANA NAZO:-
a) Uhaba wa mtaji, ambapo amekuwa na wakati mgumu wa kumiliki vifaa vya kuongeza uzalishaji, na
b) Mabadiliko ya Hali ya hewa/Tabianchi ambapo yameathiri ukanda huu na kusababisha upungufu mkubwa wa uzalishaji wa Asali.
NA HAPA ANATUELEZA MIPANGO YAKE YA BAADAE:-
"Mipango yangu hapo siku za usoni ni kuboresha shuhuli za ufugaji kwa kujenga banda na kuingiza mizinga yote humo ili kurahisisha uvunaji wa chavua kuepuka usumbufu wa kuroa na mvua kwani Chavua huharibika kwa maji"
HUU NDIO WITO WAKE KWA:-
"Wafugaji wote tuungane na ili kuimarisha uzalishaji na kuwa na soko la pamoja.
na SERIKALI nayo iendelee kutuangalia na kutuwezesha zaidi hasa sisi wajasiriamali wadogo ili tupatiwe mikopo wa vifaa bora zaidi vya ufugaji wa nyuki kwa ustawi wetu na taifa kwa ujumla"
"Pia nawashauri wadau wote wapende kutumia bidhaa za nyuki kwani ni malighafi asilia na salama sana kwa mtumiaji badala ya kupenda sana bidhaa za viwandani"
Ili kutimiza azma yake mfugaji huyu tayari amesajili shamba lake kuwa shamba darasa ambalo litakuwa chini ya uratibu na ushauri wa AJE-FARMS MASHAMBA YANAYOTEMBEA ;na hivi karibuni watu wengine watafika shambani kwake kuweza kujifunza ufugaji wa nyuki kwa vitendo. Kupitia shamba darasa hili pia mfugaji huyu atapata wateja na wawekezaji shambani kwake kwa sababu mradi wa shamba darasa pamoja na malengo mengine utalitangaza shamba hili la mfano.
Fuatilia habari zaidi kutoka katika shamba hili katika makala zijazo.
Wasalaam,
Imeandaliwa na mwandishi wetu
Safina Jihadi;Mashamba Yanayotembea-Zanzibar.